Mtanzania mdogo atumia ubunifu wa kipekee kutengeneza vigae

184

Edgar2

Hata maandiko ya Biblia yanasema hakuna jambo lisilowezekana ambapo tumeshuhudia kijana mdogo mwenye umri wa miaka 17 Edgar Edmund Tarimo ameweza kubuni na kutengeneza mashine ya kutengenezea vigae vya sakafu, (Paving Blocks), kwa kutumia taka za plastiki na mchanga.

Ubunifu wake huo wa kipekee umemfanya kupunguza kiasi kikubwa cha taka za plastiki mitaani na kusaidia kupunguza uchafu wa mazingira zinazotokana na taka za plastiki.

Kijana Edgar ana kampuni yake ya Green Venture na ameajiri wafanyakazi sita na kuwavuta watu 80 ambao wanawalipa kutokana na kumkusanyia taka za plastiki.

Edgar ameanza na mtaji wa elfu 40 za Kitanzania hadi kufika millioni 4.

Kijana huyo ambaye amehitimu kidato cha nne mkoani Arusha mwaka uliopita aligundua ubunifu huo miaka mitatu iliyopita kutokana na tatizo la mafuriko lililowahi kutokea na baadhi ya watu nyumba zao zilisombwa na maji hivyo kupelekea mkusanyiko wa uchafu wa plastiki zilizosababisha mazingira kutokuwa salama.

Paving

Vigae alivyotengeza kwa kutumia taka za plastiki

“Nilifikiria jinsi ya kutatua matatizo mawili kwa suluhisho moja ndio nikafikiria jinsi gani naweza kutumia taka kutengeneza bidhaa za ujenzi ambazo zinaweza kuwa za bei rahisi ili watu watumie kujengea katika nyumba zao ziwe imara, na pia kupunguza uchafu wa mazingira kwa kukusanya taka hizo za plastiki na kuzitumia.”

Machine

Mashine maalumu anayoitumia

Kabla ya kuwa na mashine maalumu, alikuwa na jiko la mkaa na sufuria kwa lengo la kuyeyusha plastiki hizo.

Kwa upande mwingine, mama mzazi wa Edgar, Emiliana Tarimo anasema ameshangazwa na ubunifu alionayo mwanae hadi kupata mafanikio makubwa kulingana na changamoto za awali alizozipata.

Mama Tarimo ameeleza kuwa pamoja ya kwamba bado ni mdogo amemshauri aendelee na shule ili aweze kupata maendeleo makubwa zaidi na vilevile ameiomba serikali kumpa sapoti mtoto wake ili asipoteze kipaji chake.

Mwaka jana, Edgar alifanikiwa kupata tuzo ya “Anzisha Prize” baada ya wazo lake la kibiashara la kubadilisha taka za plastiki kuwa malighafi ya kutengeneza vigae (Paving Blocks) kwa mchanganyiko wa mchanga kuibuka kidedea.

Chanzo: BBC