Wanawake Kenya waandamana

90

Maandamano Kenya

Wanawake walio na hasira wameandamana leo mjini Nairobi kulalamika tuhuma za kufukuzwa kwa mwanamke mmoja kutoka mgahawa wa Olive Restaurant kwa kumyonyesha mtoto wake.

Wanawake hao wameelekea katika mgahawa wa Olive Restaurant, ambako mama huyo anatuhumu kuwa aliambiwa ajifunike wakati anamnyonyesha mtoto wake mwenye umri wa Mwaka mmoja.

Alieleza kisa kilichompata katika kundi moja la akina mama katika mtandao wa kijamii Facebook, na kusema kuwa aliambiwa akamyonyeshe mtoto wake chooni, jambo lililomuacha akihisi kudharauliwa.

Taarifa hiyo imezusha hisia kali kote nchini na kusababisha makundi ya kutetea haki za wanawake kuandaa maandamano ya leo mjini. Mgahawa huo umeomba utulivu udumishwe kufutia ghadhabu hiyo kubwa ya wanawake nchini ukiomba kupewa muda kulishughulikia suala hilo kwa undani.

Mojawapo ya mashirika yalioshiriki maandamano hayo leo ni Muungano wa mawakili wanawake FIDA. Unasema dhamira kuu ya maandamano ya leo ni kushinikiza haki za akina mama ziungwe mkono na kusaidiwa katika kufanikisha kuwanyonyesha watoto wao bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Chanzo: BBC Swahili (http://www.bbc.com/swahili)