Trillioni 40 kuwekezwa kwa viwanda 200 Tanzania

72

Standard1

Benki ya Standard Chartered ina mpango wa kuwekeza dola za Kimarekani billioni 20 (sawa na trillioni 40 za Kitanzania) katika kampeni ya China ya uwezeshaji mitaji na biashara kutoka Asia kwenda nchi nyingine za dunia.

Kampeni hiyo iitwayo One Belt One Road inagusa nchi 65, huku Tanzania ikiwa ni mmojawapo ambapo inatarajia kuwekeza katika viwanda 200 nchini kwa lengo la kutoa ajira za moja kwa moja 150,000 na zisizokuwa moja kwa moja 350,000.

Taarifa hiyo imethibitishwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Charles Mwijage katika hafla ya chakula cha jioni kwa wawekezaji kutoka China na kuandaliwa na Standard Chartered.

Bwana Mwijage ameeleza namna benki hiyo imefanya jambo la kipekee kuandaa hafla hiyo kwa wawekezaji wa China ili kutangaza fursa za ajira ambayo imekuwa changamoto kubwa mpaka sasa huku akidai Tanzania inapambana vilivyo kuingia katika uchumi unaoendeshwa na viwanda na kampeni ya China.

Aliongeza serikali inafanya kila jitihada kuweka mandhari ya uwekezaji huku akigusia zaidi uchumi unaokua kwa kasi kwa asilimia 6 mpaka 7 huku benki hiyo ikionesha fursa za uwekezaji na uendeshaji wa uchumi ambazo zinakaribishwa na serikali ya Tanzania.

Aidha hotuba ya Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Aristide Mbwasi alisema kwamba mpango huo wa China unaozungumzia uwezeshaji wa mitaji na biashara kutoka Asia kwenda nchi nyingine ni kichocheo cha kukua kwa uchumi mbalimbali duniani na kutaka watanzania kushiriki kikamilifu.

Hata hivyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo nchini Tanzania, Sanjay Rughani amesema kwamba Benki ya Standard Chartered duniani inawekeza katika Belt and road Initiative kiasi cha dola bilioni 20 sawa na shilingi trilioni 44.8 za Kitanzania kuwezesha miradi mbalimbali kwenye kampeni hiyo ya China huku akiongeza mwaka jana benki hiyo iliingia mikataba katika miradi 40 kwenye nchi mbalimbali za mradi huo.

“Standard Chartered imewekeza katika nchi 45 za kampeni ya belt and Road zenye msukumo mkubwa wa shughuli zikiwemo nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, Kusini mwa Asia na Afrika,” na kuongeza kazi kubwa ni utoaji wa fedha ikiwemo mikopo na miamala mbalimbali.